Shirika lisilo la kiserikali Resource Oriented Development Initiative (RODI) limedhamiri kusaidia kupunguza kiwango cha maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) mkoani Rukwa kutoka asilimia 6.2 ya sasa hadi kufikia asilimia 2.0 ifikapo 2015.
Mkurugenzi wa RODI mkoani Rukwa, Gideon Mpina alibainisha hayo hivi karibuni alipokuwa anazungumzia mikakati ya shirika lake katika mapambano dhidi ya Ukimwi.
RODI inatekeleza miradi ya mapambano dhidi ya maambukizi ya VVU na kutoa Elimu ya Afya ya Uzazi na Ujinsia (TMEP) kwa ufadhili wa Taasisi ya Kimataifa ya Elimu ya Afya na Uzazi kutoka nchini Sweden (RFSU) ambapo kiwango cha maambukizi ya VVU kimeripotiwa kuongezeka kutoka asilimia 4.9 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 6.2 mwaka huu.
Alizitaja mbinu zitakazotumiwa na RODI kupunguza maambukizi hayo ya VVU kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia sasa zikiwemo kusambaza kondomu na kutoa elimu sahihi ya matumizi yake pia kuwaelimisha wakazi wa mkoani humo umuhimu wa tohara kwa wanaume.
Alibainisha kuwa kiwango cha maambukizi wilayani Sumbawanga kinatisha ambapo kiwango cha maambukizi katika Mji Mdogo wa Laela na Mji wa Mpui wilayani humo ni asilimia 10 kila mmoja.
Kwa mujibu wa takwimu za Afya mkoani Rukwa, kiwango cha maambukizi ya VVU Manispaa ya Sumbawanga kimefikia asilimia 5.2.