Wizara ya Uchukuzi imesaini mkataba na Uholanzi kwa ajili ya kuongeza wigo wa safari za ndege baina ya nchi hizo (BASA) kukabili changamoto za usafiri wa anga pamoja na kuongeza ulinzi na usalama wa anga.
Mkataba huo ulisainiwa jana Dare s Salaam kati ya Waziri wa wizara hiyo, Dk Harrison Mwakyembe na Balozi wa Uholanzi nchini, Jaap Frederiks.
Akizungumza baada ya kutia saini mkataba huo, Dk Mwakyembe alisema makubaliano hayo yataweza kutoa fursa nzuri kwa wasafiri wa nchi hizo pamoja na mizigo.
Alisema hiyo ni fursa kwa mashirika mengine kati ya nchi hizo kujitokeza na kutoa huduma kwa kuongeza idadi ya safari. Pia kutakuwa na ushindani wa nauli pamoja na kuongeza vituo na kulinda haki za abiria.
Kwa mujibu wa Waziri, ndege zinazofanya safari katika nchi hizo zitatua katika viwanja vya Songwe na Mwanza tofauti na awali ambapo walitumia vituo vya Zanzibar, Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere (Dar es Salaam) na Mwanza.
Dk Mwakyembe alisema awali makubaliano kama hayo yaliwahi kufanyika mwaka 1978 ambapo masuala ya anga yalikuwa na upeo mdogo.
Balozi Jaap alisema soko la Tanzania limekuwa likikua, ikiwa ni pamoja na sekta ya usafiri ambalo ni eneo maalum la kukuza utalii na biashara.