Aliyekuwa katika tukio la uporaji wa Sh milioni 20 kutoka kwa mtumishi wa duka la kubadilishia fedha za kigeni la Northern Bureau de Change, ametambuliwa kuwa ni mwalimu mstaafu wa jijini Arusha, Benedict Mmasi.
Mmasi ambaye mkewe ni Diwani wa Viti Maalumu, Liliani Mmasi (CCM), aliuawa juzi.
Alipigwa risasi baada ya kutoka kusali katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Mjini Kati na kwenda kununua magazeti eneo ambako uporaji ulifanyika.
Alipoona mama akipiga kelele kuomba msaada, Mmasi alikwenda kusaidia lakini kabla ya kufika alipigwa risasi ubavuni na kufa papo hapo . Ilikuwa saa 3.30 asubuhi katika Mtaa wa Maeda katikati ya Jiji la Arusha. Majambazi hao walikuwa kwenye pikipiki na walikimbia kupitia barabara ya Old Moshi.
Kwa mujibu wa kaka wa marehemu, Adamu Mmasi kifo cha mdogo wake kimeacha pengo kubwa kwa familia. Ameacha mke, Liliani na watoto watatu; wawili wakiwa wa kike.
Kaka huyo wa marehemu alisema ndugu yake kabla ya kujishughulisha na biashara ya kununua, kuuza na kuchimba madini, alifundisha shule kadhaa jijini hapa.
Maziko yatafanyika keshokutwa nyumbani kwake Mashono jijini hapa.