Serikali imeonya makandarasi wenye tabia ya kuhonga watumishi wa Serikali ili wapatiwe zabuni za ujenzi wa miradi mbalimbali kuacha mara moja.
Onyo hilo lilitolewa mwishoni mwa wiki na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Musa Iyombe, wakati akifunga mkutano wa mwaka wa siku mbili ulioandaliwa na Bodi ya Makandarasi (CRB), ulioshirikisha zaidi ya makandarasi 900.
"Baadhi yenu mnaenda kwa mameneja wa mikoa wa Tanroads (Wakala wa Barabara) mnaahidi kutoa rushwa mpate zabuni, hamuwatendei haki wenzenu, acheni tabia hiyo ili kazi zitolewe kwa haki na kila mtu apate haki yake wakati zabuni zinapotangazwa," alisema.
Alisema, "Mkandarasi anamwambia meneja wa mkoa kuna kazi naitaka nikiikosa ile nitakufa, nikiipata ile kazi nitakuona mimi niliwahi kuwa Meneja wa Mkoa kwa hiyo najua mnavyowashawishi watumishi wa Serikali ili mpate zabuni na tabia hiyo ife ili haki isinunuliwe."
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick aliwataka makandarasi kukamilisha miradi kwa wakati na kwa ubora wa hali ya juu na kuachana na visingizio vya malipo madogo ya miradi ya ujenzi.
Alisema kuna baadhi ya makandarasi ambao wamekuwa wakisuasua katika ujenzi wa miradi wanayopewa na kuishia kutoa visingizio vya kucheleweshewa malipo ama zabuni kutolewa kwa fedha kidogo.
"Kama fedha za mradi ni kidogo kwa nini ulikubali kuifanya hiyo kazi, mwingine kazi ya miezi mitatu anafanya miaka miwili sasa hapo unachelewesha kupatikana huduma iliyokusudiwa, kama hi zahanati ina maana watu wanakosa tiba kwa uzembe wako," alisema.
Mwenyekiti wa Bodi ya CRB, Consolata Ngimbwa, alisema makandarasi wanapaswa kuimarisha vyama vyao viwe na nguvu na sauti ya kusemea wanapopata matatizo kwenye kazi zao.
"Vyama vyenu ni dhaifu sana na hilo linatokana na wengine kutokuwa wanachama wa vyama hivyo, nitasimamia kuanzishwa kwa sheria itakayomlazimisha kila mkandarasi kujiunga na vyamaa vyenu na ninawaahidi hilo nitalisimamia kuanzia wiki ijayo," alisisitiza Ngimbwa.