Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Mathew Sedoyeka amepongezwa na vijana wilayani humo kwa uamuzi wake wa kuwapiga marufuku vijana wote wa kiume popote wilayani humo kuvaa suruali kwa mtindo wa mlegezo maarufu kama Kata K .
Hata hivyo wamemtaka DC huyo apige marufuku wasichana kuvaa mavazi yasiyo ya staha ikiwemo vipedo na sketi fupi huku baadhi yao wakiwa nusu uchi kwamba uvaaji huo nao pia hauendani na maadili ya Watanzania.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wa habari hizi baadhi ya vijana wa kike na kiume wamemtaka Mkuu huyo wa Wilaya, kuamuru kuwa kijana yeyote akikamatwa amevaa mavazi hayo yasiyo na stahi awe wa kike au wa kiume atozwe faini ya kiasi cha Sh 50,000 na fedha hiyo apewe mtu aliyemkamata na kufikishwa Kituo cha Polisi.
"Kwa staili hii ya kupigwa faini itatuogopesha na nikuhakikishie tutaacha tabia hii ya kuvaa kiajabu ajabu," alisema Tofilo Mbalamwezi, mkazi wa eneo la Majengo.
Kauli na pongezi hizo za vijana hao zimekuja siku chache baada ya DC kupiga marufuku uvaaji wa suruali kwa staili ya Kata K kwa kijana yeyote wa kiume mahali popote wilayani humo.
Pia Sedoyeka aliwaagiza viongozi wa serikali za mitaa, vijiji, kata tarafa na wilaya kushirikiana na Kamati za Ulinzi na Usalama katika maeneo yao ya kiutawala kuwachukulia hatua kali vijana wote wa kiume watakaobainika kuvaa suruali zao kwa staili hiyo ya Kata K.
Alitoa maagizo hayo hivi karibuni akihutubia mikutano mbalimbali ya hadhara wilayani humo ambapo alisema tabia hiyo ya vijana wa kiume kuvaa suruali zao kinyume cha utaratibu haiwezi kuvumilika kwa kuwa inatukanisha jamii.