Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika imewaomba wadau wa sekta ya sukari nchini wakiwemo wazalishaji katika viwanda vya ndani kuendelea kutoa
ushirikiano wa karibu na vyombo vya dola kwa kuhakikisha wanawafichua wafanyabiashara wasio waaminifu wanaoingiza sukari kwa njia ya magendo.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Wizara hiyo , Godfrey Zambi, wakati akizungumza na Menejimeti ya Kiwanda cha Sukari Kilombero , juzi.
Naibu huyo alifanya ziara ya kuangalia hali ya uzalishaji wa sukari na kupata changamoto kutoka kwa Uongozi wa kiwanda hicho.
Hata hivyo alisema, licha ya viwanda vya ndani kutokuwa na uwezo wa kukidhi mahitaji ya sukari nchini, na kuifanya Serikali kulazimika kuziba
pengo hilo kwa kuagiza sukari toka nje , hatua hiyo isitumike visivyo na wafanyabiashara hao kwa kukiuka utaratibu uliowekwa kisheria.
“ Katika kudhibiti jambo hilo ,TRA imepewa kazi hiyo
kuona na kuhakikisha sukari inayoingia kwa magendoinadhibitiwa na pia inayosafirishwa inakuwa chini ya uangalizi maeneo yote” alisema Naibu Waziri.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri huyo, TRA pia imepewa jukumu la kupitia upya sheria ya kodi kwa bidhaa hiyo inayoagizwa kutoka nje ili bei yake isiweze
kuathiri ushindani wa soko kutoka viwanda vya hapa nchini.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda cha Sukari Kilombero, Joseph Rugaikamu alitoa taarifa ya hali ya uzalishaji wa sukari kwenye kiwanda hicho alisema hadi kufikia Mei 17, mwaka huu kilikuwa na tani za sukari 24,999 zilizokosa soko.
Naye Meneja Maendeleo Mipango na Uratibu wa Bodi ya Sukari nchini, Abdul Mwamkemwa ,alisema katika kudhibiti uingizaji wa sukari na magendo na kutolipiwa kodi , Mamlaka ya Mapato Tanzania ( TRA ), ndio wenye jukumu la kusimamia na tayari wamebuni njia mbadala ya kudhibiti hali hiyo ambayo itaondoa hali inayojitokeza kwa sasa.