Quantcast
Channel: ziro99blog
Viewing all articles
Browse latest Browse all 4561

WALIMU WALAZIMISHWA KUKAA SAKAFUNI MBELE YA WANAFUNZI WAO...

$
0
0
Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, kimelalamikia kitendo cha  Ofisa Elimu wa Wilaya hiyo, Josephat Maganga kudaiwa kudhalilisha walimu wa shule ya msingi ya Nyamoko katika mkutano wa hadhara.
Akizungumza jana kwa njia ya simu, Mwenyekiti wa Chama hicho, John Magoko alisema Ofisa huyo alidhalilisha walimu hao kwa kuwataka wakimbie kuzunguka shule na kuwaamuru wakae chini katika mkutano ulioitishwa na wanakijiji.
Alisema wanakijiji hao walikuwa wanamtuhumu Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Amani Mgunda, kutumia Sh 740,000 za shule, hivyo kuitisha mkutano huo kwa lengo la kuhoji matumizi ya fedha hizo na kutaka walimu wote kuhudhuria.
Hata  hivyo, hakuna mwalimu aliyehudhuria mkutano huo ndipo Maganga alipokwenda katika nyumba za walimu zilizo karibu na shule na kuwataka watoke haraka waende kwenye mkutano huo.
“Aliwaamuru wakimbie, kisha wakae chini kwenye mkutano huo uliohudhuriwa na watu wengi wakiwamo pia wanafunzi wao, akaendelea kutoa maneno ya kashfa kuwa atawahamisha wote, kwa sababu hawana adabu na wana kiburi,” alisema Magoko.
Kutokana na kitendo hicho walimu walilalamika kudhalilishwa mbele ya wanafunzi na wanakijiji kwenye mkutano huo, na wengine wamegoma kuingia madarasani kwa siku mbili wakiomba kuhamishwa kituo cha kazi.
 “CWT tunalaani kitendo  hiki cha udhalilishaji wa taaluma yetu, tunamwomba Maganga aombe radhi walimu hao ili waendelee na kazi kwa kuwa wengi wanafika kazini lakini hawaingii madarasani kufundisha,” alisema.
Aidha, alisema walizungumza na Maganga ambaye aliahidi juzi kukutana na walimu ili awaombe radhi vinginevyi au wasipokubaliana watakwenda kumwona Mkurugenzi wa Halmashauri.
Akielezea tukio hilo jana Maganga alisema Jumatano, alipigiwa simu kuwa wanakijiji wanataka kuchoma nyumba ya Mwalimu Mgunda, akaomba polisi  waende naye ili kuzungumza na wanakijiji hao, lakini walimu hawakuhudhuria   kikao hicho.
Maganga alisema aliagiza polisi waite walimu wote, lakini waligoma ndipo alipowafuata na kuwaamuru wakimbie kwenda kwenye kikao hicho cha dharura ili kuokoa maisha ya mwalimu huyo na kuboresha uhusiano baina yao na wanakijiji.
“Hakuna mwalimu aliyepigwa wala kurushwa kichura, bali walipogoma kuja nilikasirika nikawafuata na kuwaamuru wakimbie kuwahi mkutano kwa sababu kuna tukio la dharura,” alisema.
Hata hivyo, alisema tayari amezungumza nao na wamekubali kuwa hali hiyo ilikuwa ya dharura na wamechukua hatua dhidi ya Mwalimu Mgunda aliyesababisha tukio hilo, kwa kutoa taarifa za uongo kwa wananchi.
Juhudi za kumpata Mwalimu Mgunda azungumzie tuhuma hizo hazikufanikiwa kutokana na simu yake kupigwa lakini ikawa haipatikani.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 4561

Trending Articles