Quantcast
Channel: ziro99blog
Viewing all articles
Browse latest Browse all 4561

MZINDAKAYA AULIPUA UMOJA WA KATIBA YA WATANZANIA BUNGENI

$
0
0
Mwanasiasa mkongwe nchini,  Dk Chrisant Mzindakaya ameutupia kombora Umoja wa Katiba ya Watanzania - nje ya Bunge Maalumu (Ukawa-nje) kwa kuzungumzia mjadala wa katiba nje ya Bunge Maalumu na kuita kitendo hicho kuwa ni uhaini wa kisiasa.

Dk Mzindakaya alisema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam juu ya mchakato wa Katiba mpya unaoendelea bungeni mjini Dodoma.
“Uamuzi wa Ukawa kuendeleza mazungumzo nje ya Bunge ni uhaini wa kisiasa na hawana uhalali wa kudai kuwa wanawawakilisha Watanzania wote,” alisema Mzindakaya.
Kauli ya mwanasiasa huyo ambaye pia amehoji juu ya takwimu zilizotolewa na Tume ya Marekebisho ya Katiba zikidai watu wengi walitaka muundo wa serikali tatu, imekuja siku chache baada ya baadhi ya watu wakiwemo viongozi wa dini pia kukaririwa hivi karibuni na gazeti hili wakikosoa umoja huo.
Walishutumu umoja huo nje ya Bunge maalumu wakisema hatua yake ya kutaka kuzunguka nchi nzima ni kutumia muda na rasilimali vibaya.
Hivi karibuni Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Willibrod Slaa kwa niaba ya makatibu wakuu wa vyama vya upinzani vinavyounda Ukawa  ndani na nje ya Bunge Maalumu la Katiba, alisema Ukawa-nje imeundwa kushawishi wananchi nchi nzima  kudai katiba yenye maslahi yao.
Kwa mujibu wa Dk Slaa, miongoni mwa ajenda kuu za Ukawa-nje  ni kuhakikisha wanaelimisha wananchi mambo yote wanayopaswa kuelewa kuhusu mchakato unaoendelea ili wakati wa kupiga kura ya maoni kukubali au kukataa Katiba itakayopendekezwa, wawe na uelewa mpana. Elimu hiyo wanaitoa kwa njia ya mikutano ya hadhara nchi nzima na hivi karibuni walikuwa Mwanza.
Wakati huo huo, Mzindakaya amekosoa wanaolalamikia hotuba ya Rais Jakaya Kikwete kwenye Bunge Maalum la Katiba mjini Dodoma hivi karibuni akisema, ilikuwa ni dira  ya kusaidia wananchi kuelewa na wakati huo huo wabunge kusoma rasimu hiyo na kuichambua kwa kina  hatimaye, waijadili na kufikia muafaka utakaoleta manufaa kwa taifa na vizazi vijavyo.
Alisema rais alikwenda kuhutubia bunge kusaidia kueleza mambo ya manufaa kwa wananchi. Alikosoa kwamba mwanasiasa aliyekuwa kwenye Tume au ambaye hakuwa kwenye tume,  kusimama bungeni na kusema Bunge lizingatie na kupitisha rasimu fulani kwa maana kwamba, ndiyo maoni ya wananchi,  anapotosha.
Mzindakaya alifafanua tume haikufanya kazi ya kukusanya maoni kuhusu muundo wa serikali mbili au tatu, bali ilikusanya maoni ya jumla ya wananchi namna  katiba mpya itakavyokuwa.
“Tume ingefanya kazi ya kukusanya maoni ya wananchi kuhusu muundo wa serikali mbili au tatu, tungepata msimamo wa wananchi, sasa hatujafika huko,” alisema na kusisitiza, maelezo aliyotoa Rais hata yaliyomo ndani ya tume yanaonesha kuwa watu waliokutana na tume ni 300,000  na kati ya hao, waliotoa maoni kuhusu muundo wa Muungano kwa maana ya serikali tatu walikuwa asilimia 24 pekee.
Kwa mujibu wa Mzindakaya, hata wale wengi kati ya hao 300,000, hawakusema wanataka muundo wa serikali tatu.
“Hizi ni taarifa zinazopotosha na ndiyo maana Rais Jakaya Kikwete alitoa takwimu bungeni ili kusaidia wabunge na wananchi kuelewa na kuwaonya wanasiasa wanaong’ang’ania kusema ni maoni ya wananchi, wanakosea.”
Mwanasiasa huyo mkongwe nchini pia amemtetea Profesa Issa Shivji  dhidi ya wanaomwandama baada ya kukaririwa hivi karibuni akitetea muundo wa muungano wa serikali mbili.
Alimtaja Shivji kuwa miongoni mwa wasomi wazalendo waliojizolea sifa kubwa nchini katika nyanja za elimu, uzoefu katika uchambuzi wa  mambo mbalimbali ya ndani na nje kimataifa.
“Ukimwandama Profesa  Shivji kwa sababu yeye anazungumzia habari ya serikali mbili, na kwa kurejea huko nyuma kwamba yeye alikuwa hapendi serikali mbili, tutauliza vile vile wanasiasa ambao wameishi na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere miaka yote na serikali mbili mpaka imefika miaka 50 na alikuwa madarakani na wao waliona na walisaidia kuimarisha kwa kuwa na sheria na katiba ya serikali mbili….
“Tutasemaje pia kama leo hii mtu huyo huyo aliyetaka serikali mbili leo anataka tatu, kwa nini tumponde Profesa  Shivji yeye anayependekeza serikali mbili si kwa kutumiwa katika usomi wake ambao hawezi kumtumia kwani ana msimamo thabiti na kama angependekeza serikali tatu asingelaumiwa,” alisema.
Aidha, Mzindakaya alisema tatizo lililopo kwa upande wa Zanzibar, ni kwamba wapo viongozi wanaoendelea kuwa na  kasumba ya utawala wa kikoloni ulioondolewa.
“Kuna mawakala wa wakoloni ambao wangetaka kurudi kwa mfumo wa ukoloni mamboleo kule visiwani. Kinachoudhi zaidi ni kuwa baadhi ya mawakala  wanaotetea muundo wa serikali ya mkataba, serikali tatu ni wachovu wamekwishakuwa wazee …,” alisema.
Hata hivyo mwanasiasa huyo mkongwe, alisema anaamini Bunge Maalumu la Katiba litafanya vizuri chini ya uongozi wa Mwenyekiti wake, Samuel Sitta.
Alitoa mwito kwa wananchi akisema hakuna haja ya kufadhaika kwa sababu wajumbe wanaelewa wanachokifanya  bungeni  ipatikane katiba  yenye maslahi kwa taifa.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 4561

Trending Articles