Quantcast
Channel: ziro99blog
Viewing all articles
Browse latest Browse all 4561

KAMATI ZA BUNGE MAALUMU LA KATIBA ZALALAMIKIA UFINYU WA MUDA...

$
0
0
Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta.
Asilimia kubwa ya Kamati 12 za Bunge Maalumu la Katiba, zimedai muda  uliotolewa kujadili sura mbili hautoshi, hivyo zinatarajia kuomba kuongezewa, zikamilishe.

Kamati  hizo 12 zilianza tangu juzi kujadili   Sura ya Kwanza na ya Sita za rasimu hiyo na zilitakiwa kukamilisha kazi hiyo kabla ya leo.
Miongoni mwa kamati ambazo wenyeviti wake walizungumza na waandishi wa habari mjini hapa,  ni Kamati namba 5 inayoongozwa na Hamad Rashid Mohamed, ambayo jana ilikuwa imekamilisha kujadili Ibara zote 9 za Sura ya Kwanza ya Rasimu ya Katiba mpya na kubakiwa na Sura ya Sita.
Kwa mujibu wa Hamad, hadi jana mchana, Kamati yake ilikuwa haijaanza kujadili Sura ya Sita inayohusu Muungano na alisema kanuni ilikuwa imetoa muda mfupi wa mjadala ambao ni siku mbili na hivyo kuhitajika kuomba Bunge kuongeza muda zaidi.
Akizungumzia Sura ya Kwanza, alisema kulikuwa na utata mkubwa kuhusu tafsiri ya aina ya Muungano kwenye hati, alisema ulimalizwa na Mwanasheria wa zamani wa Jamhuri ya Muungano, Andrew Chenge.
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo wa kamati, Chenge alifafanua kuwa  ni Muungano wa nchi mbili na si Shirikisho.
Akizungumzia Ibara zilizopitishwa na kukataliwa, Hamad alisema wajumbe wa Zanzibar walitimiza idadi ya kura ya theluthi mbili na kupigia kura ya kukataa Ibara hiyo huku Tanzania Bara wakishindwa kufikia  theluthi mbili ya wapiga kura na kukosa sifa ya kupigia kura Ibara hiyo.
Ibara hiyo inasema Tanzania ni nchi na Shirikisho lenye mamlaka kamili ambalo linatokana na Muungano wa nchi mbili za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.
Kwa upande wa Ibara namba mbili inayohusu eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hamad alisema pande zote mbili zilitimiza ikama ya theluthi mbili ya wapiga kura na pande zote ziliikataa.
Alisema kwa Ibara namba tatu inayohusu alama na Sikukuu za Taifa, wajumbe waliikubali, Ibara namba nne inayohusu lugha za Taifa na lugha za alama wajumbe walikubali, Ibara namba tano inayohusu tunu za Taifa wajumbe walishindwa kutimiza idadi ya kura.
Ibara namba sita, Hamad alisema inayohusu Mamlaka ya Wananchi, Utii na Hifadhi ya Katiba na wajumbe wa pande zote waliikubali.
Kuhusu Ibara namba saba inayohusu Watu na Serikali, wajumbe waliikataa, Ibara namba nane inayohusu Ukuu na Utii wa Katiba wajumbe waliikubali wakati Ibara ya Tisa inayohusu Hifadhi ya Utawala wa Katiba wajumbe waliikubali.
"Kamati yetu imeweza kufanya kazi nzuri  sana pamoja na tofauti zilizojitokeza. Sisi tuliweza kuelewana na hatukwenda mbali sana kabla ya kufikia maelewano," alisema Hamad.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati Namba 2, Shamsi Vuai Nahodha alisema kamati yake hadi jana, ilijadili  sura zote mbili, isipokuwa walibakisha kupiga kura ya kupitisha ibara.
"Kama hadi saa 2:30 usiku (jana) tutakuwa hatujamaliza, tutaomba tuongezewe muda na Mwenyekiti wa Kamati," alisema.
Kwa mujibu wa maelekezo ya  Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba,  Samuel Sitta, kwa wajumbe, kazi  ya kuchambua sura  hizo mbili ilitakiwa kufanyika juzi na jana.
Leo inatakiwa iwe siku maalumu kwa Kamati ya Uandishi, kufanya kazi yake ya  kuandika masuala yaliyojadiliwa na kuafikiwa au kutoafikiwa na wajumbe walio wengi.
Iwapo kamati zitakuwa zimekamilisha kazi na kuiwasilisha kwa Kamati ya Uandishi, Ijumaa,  wenyeviti wa kamati hizo 12 wanapaswa kuwasilisha taarifa zao bungeni kwa mjadala.
Hata hivyo baadhi ya wajumbe walisema upo uwezekano kesho bunge litakapokaa, ndipo Mwenyekiti atatumia nafasi hiyo kutangaza kuongeza muda kwa kamati ambazo zitakuwa hazijakamilisha kazi yake.
Hata hivyo mwandishi hakufanikiwa kumpata ama  Mwenyekiti au Katibu wa Bunge Maalumu kwa ajili ya kufafanua utaratibu wa kuongeza muda kazi hiyo ya kujadili sura mbili ikamilike.
Sitta alisema Kamati ya Uongozi ya Bunge Maalumu, iliamua kuanza kujadiliwa kwa sura namba moja na sita, kutokana na sura hizo kuwa na mambo yanayofanana kuhusu muundo wa Serikali na Muundo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kupatikana kwa muundo kumeelezwa na Mwenyekiti  huyo, kutafanya mjadala juu ya masuala mengine kuwa rahisi.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 4561

Trending Articles