Quantcast
Channel: ziro99blog
Viewing all articles
Browse latest Browse all 4529

MAGARI MITUMBA, MATAIRI CHAKAVU CHANZO CHA AJALI ZA BARABARANI 4,553...

$
0
0
Mafundi wakibadili moja ya magurudumu ya lori.
Ununuzi  wa magari  nje ya nchi yaliyokaa muda mrefu kisha kuyatumia nchini,  unadaiwa kuchangia ajali nyingi barabarani, kutokana na baadhi tairi kuisha muda wa matumizi.
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeshauri wanunuzi kuhakikisha wanabadili vipuri, hususan tairi baada ya kuingiza magari, kwa lengo la kupunguza wimbi la ajali za mara kwa mara.
Kauli hiyo ya Mkuu wa Maabara ya Uhandisi na Mitambo wa TBS, Clarence Haule imekuja siku chache baada ya kutokea ajali tofauti   mkoani Kilimanjaro na Pwani zilizosababisha jumla ya vifo vipatavyo 30.
Wimbi la ajali za barabarani limethibitishwa pia na takwimu zilizotolewa jana Dar es Salaam na Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani.
Takwimu hizo zinaonesha vifo  829 vimeripotiwa kuwepo katika miezi mitatu kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu, vikitokana na ajali 4,553 za barabarani zilizotokea katika kipindi hicho.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana Dar es Salaam, Mkuu wa Maabara ya Uhandisi na Mitambo wa Shirika la Viwango nchini (TBS), Clarence Haule alisema gari linaweza kuwa jipya lakini tairi zikawa zimekwisha muda wake.
Hata hivyo, alisema zipo sababu nyingi zinazochangia ajali ikiwemo mwendo kasi. Alisema tatizo kubwa liko pale ambapo mnunuzi hununua gari lililokaa muda mrefu, ambao ni zaidi ya miaka mitano huku akiendelea kutumia tairi alizonunua nazo.
“Mara nyingi wanunuzi wa magari wanaponunua magari  huendelea kuyatumia bila kubadili tairi jambo ambalo huwa hatari na kuchangia kutokea kwa ajali,” alisema Haule na kuongeza kuwa TBS inapokagua ubora wa vipuri na magari yanayoingizwa hukumbana na suala kama hilo.
Alisema wanapokuwa wakikagua, gari likikutwa na vipuri ambavyo vimeisha muda wake, mnunuzi huelezwa na kutakiwa kubadili kabla ya kuendelea kutoa huduma.
Haule alisema tairi kama kipuri kimojawapo cha gari, lina vitu vingi vya kuangalia na lazima mnunuzi kuzingatia ubora wake anaponunua gari.
Kuhusu sababu nyingine zinazoweza kuchangia kutokea kwa ajali, Msemaji wa TBS, Rhoida Andusamile alisema ubovu wa barabara pamoja na utelezi hususani wakati wa mvua.
Alitaja sababu nyingine kuwa ni mwendo kasi wa mabasi, ujazo uliopitiliza wa abiria, uzito wa mizigo  na kutumika kwa tairi ambazo zimemaliza muda wake wa kuendelea kutumiwa.
Takwimu za polisi
Kwa mujibu wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, vifo  829 vimeripotiwa kuwepo katika miezi mitatu kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu, vikitokana na ajali 4,553 za barabarani zilizotokea katika kipindi hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari  jijini Dar es Salaam jana, Kamanda wa Kikosi  hicho, Mohamed Mpinga alisema, mwaka jana, kati ya Januari na Machi,  zilitokea ajali 5,556 vifo 861 na majeruhi 4,788.
"Mwaka huu kuna upungufu wa matukio 1,003 sawa na asilimia 18, vifo 32 sawa na asilimia 3.7 na majeruhi 792 sawa na asilimia 16.5, na kwa Mkoa wa Dar es Salaam ndio mkoa ambao unaongoza kwa ajali hizo," alisema Kamanda Mpinga.
Mpinga alitaka madereva kuwa makini hususani kipindi hiki cha mvua, ambacho madaraja mengi yameharibika, barabara zina mashimo na pia upo utelezi mwingi barabarani.
Hata hivyo Polisi  Kikosi cha Barabarani imesema  upo upungufu mkubwa wa ajali na vifo vya ajali za barabarani nchini ikilinganishwa na mwaka jana, ambao katika kipindi kama hicho (miezi mitatu), kulikuwa na vifo vya watu 861.
Kwa upande wake,Msemaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra),  David Mziray alisema madereva wa mabasi wanatakiwa kuwa waangalifu hususani kipindi  cha mvua.
Kuhusu  hatua zinazochukuliwa kwa mabasi ambayo ni kinara kwa kusababisha ajali, alisema hufungiwa kwa wiki mbili hadi tatu, kuwawezesha kubadilika na kufanya kazi yao kwa weledi.
Alisema mabasi yanapofungiwa, hukaguliwa na kikosi cha Sumatra kuweza kubaini kiini cha kusababisha ajali za barabarani.
Hivi karibuni, kumetokea mfululizo wa ajali za barabarani zilizosababisha vifo vya zaidi ya watu 30. Katika ajali hizo, watu 22 walikufa katika ajali ya gari iliyotokea katika Kijiji cha Mkupuka Tarafa ya Kibiti,  ikihusisha magari matano.
Kadhalika watu 12 walikufa, 10 kati yao  papo hapo, baada ya ajali iliyotokea eneo la Hedaru, Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro na kuhusisha magari matatu.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 4529

Trending Articles