Quantcast
Channel: ziro99blog
Viewing all articles
Browse latest Browse all 4576

UCHAMBUZI MUUNDO WA MUUNGANO KUFANYIKA LEO NA KESHO...

$
0
0
Wajumbe wakifuatilia moja ya vikao vya Bunge la Katiba.
Muundo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umeanza kujadiliwa rasmi kupitia Kamati 12 za Bunge Maalumu la Katiba ambazo zinajadili  Sura ya Kwanza na ya Sita za rasimu ya Katiba mpya.

Kutokana na kazi hiyo, jibu la ama Tanzania kuwa na mfumo wa Serikali tatu kama ilivyopendekezwa kwenye rasimu ya pili ya Katiba iliyowasilishwa bungeni hapo na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba wiki mbili zilizopita,  au aina nyingine ya muundo, litapatikana Ijumaa.
Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba,  Samuel Sitta aliwaambia wajumbe wa Bunge hilo jana kwamba kazi hiyo ya kuchambua sura  hizo inafanyika leo na kesho. Hata hivyo alisema kazi hiyo ingeweza kuanza kufanyika jana kwa kamati ambazo zilikuwa tayari kufanya hivyo.
Alisema siku ya jana haikuhesabika kama siku rasmi ya mjadala kutokana na kuwepo shughuli nyingi za kiutawala.
Miongoni mwa shughuli hizo ni pamoja na wajumbe kuelekezwa juu ya mfumo wa mjadala kwenye kamati na pia muundo wa uandishi wa sura hizo kuweka mfumo ambao hautaleta tabu katika uandishi wa Katiba mpya.
Kutokana na hali hiyo, Sitta alisema sura hizo zitajadiliwa kwa siku mbili hadi kesho na Alhamisi itakuwa maalumu kwa Kamati ya Uandishi kufanya kazi yake ya  kuandika masuala yaliyojadiliwa na kuafikiwa au kutoafikiwa na wajumbe walio wengi.
Ijumaa,  wenyeviti wa kamati hizo watawasilisha taarifa zao bungeni kwa mjadala.
Sitta alisema Kamati ya Uongozi ya Bunge Maalumu iliamua kuanza kujadiliwa kwa sura namba moja na sita kutokana na sura hizo kuwa na mambo yanayofanana kuhusu muundo wa Serikali na Muundo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kupatikana kwa muundo kumeelezwa na Mwenyekiti  huyo kwamba  kutafanya mjadala juu ya masuala mengine kuwa rahisi.
"Kama mnavyojua sura namba moja, sura namba sita na sura namba nane zina masuala yanayofanana. Lakini kwa vile  kanuni zinatutaka tujadili sura mbili mbili tutaanza na sura namba moja na sura namba sita ambazo zinafanana maana zinazungumzia muundo wa Jamhuri na Muungano.
"Kamati zitakapojadili kuhusu muundo wa Serikali ya Jamhuri na Muungano masuala kama mahakama, dola na mengineyo yatakuwa rahisi kuyaingiza katika rasimu kwa kuzingatia mfumo utakaokuwa umekubaliwa na wajumbe wengi wa Bunge la Katiba," alisema Sitta.
Hadi ilipowasilishwa kwenye Bunge Maalumu la Katiba, rasimu ya pili ilikuwa na muundo wa serikali tatu, muundo ambao umepata upinzani mkubwa kutoka kwa wadau mbalimbali, kikiwemo Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho kimeweka msimamo wa kutaka serikali mbili katika muundo wa Katiba mpya.
Pamoja na misimamo ya vyama na wadau wengine, hata hivyo ni wajumbe pekee wa bunge hilo ndiyo wenye uwezo wa kupunguza, kuongeza au kufuta kabisa kipengele chochote kwenye rasimu hiyo ya katiba kwa namna watakavyoona inafaa.
Uamuzi huo unategemewa kufanyika kupitia mijadala ya kwenye Kamati na baadaye uamuzi utakaopitishwa na Bunge zima kupitia mfumo wa kura za siri na wazi kulingana na matakwa ya kila mjumbe baada ya mjadala.
Katika hatua nyingine, Bunge Maalumu la Katiba jana limesitisha azma yake ya kuwasilisha marekebisho ya kanuni kama ilivyotangazwa Ijumaa, huku Mwenyekiti Sitta akisema hatua hiyo inatokana na Watanzania kuchoka kusikia wimbo wa kanuni ukiimbwa kila siku bungeni.
"Watanzania wamechoka na mjadala wa kanuni kila siku, hivyo nimesitisha ratiba ya uwasilishaji wa marekebisho ya kanuni na badala yake sasa tutaanza kazi ya kujadili rasimu kwenye Kamati. Kama kuna mgongano wowote wa kikanuni utajitokeza huko mbele tutaangalia namna nzuri ya kuutatua," alisema Sitta.
Wajumbe mbalimbali wa Bunge Maalumu la Katiba, akiwemo Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Nancy Mrikaria wameendelea kukosoa mfumo wa Muungano wa Serikali tatu wakisema unabeba maslahi ya watu wachache.
Akizungumza na mwandishi jana mjini Dodoma, Mrikaria alisema  wajumbe hao wameaminiwa na wananchi na wanapaswa kuangalia  maslahi ya taifa na kuweka kando itikadi za kisiasa.
Aliasa wajumbe kuacha kung'ang'ania serikali tatu akisema serikali mbili bado zinafaa.
"Tusiangalie serikali itakayobeba maslahi ya watu wachache, cha muhimu ni kuangalia serikali yenye maslahi ya watu wengi," alisema.
Wakati huo huo, alishutumu makundi yaliyozuka ya Ukawa na Tanzania Kwanza akisema haoni kama yana msaada wowote zaidi ya fujo na kuzomeana.
"Ni tatizo kubwa kukwamisha mchakato kutokana na mivutano, ni muhimu kila mmoja angeangalia maslahi ya taifa badala ya kuangalia itikadi za vyama," alisema Mrikaria.
Mjumbe mwingine wa Bunge Maalumu, William Ngeleja amesema  upo umuhimu wajumbe wa bunge hilo kufanya maamuzi ya kuimarisha muungano na kuacha kuwa na maslahi binafsi yenye lengo la kuvunja muungano.
Alisema hayo jana mjini hapa huku akisisitiza kuwa muumini wa serikali mbili.
Ngeleja alisema msingi muhimu wa rasimu ni makubaliano hivyo ni muhimu wajumbe wakafanya uamuzi utakaoimarisha muungano licha ya rasimu kutamka serikali tatu.
"Tubishane na tujadiliane kwa hoja, tunaamua hatma ya Watanzania tutimize wajibu wetu kwani wakati wa kujadili rasimu tutaangalia mambo ya kiasiasa na kisheria pia," alisema Ngeleja.
Alisema bado serikali mbili zinafaa na jambo la muhimu ni kuangalia changamoto zilizopo na kupatiwa ufumbuzi badala ya kufikiria kuwa na serikali tatu.
Alisema kwenye kundi la watu 600 kusitegemewe kuwa na mawazo ya aina moja. Alisihi Watanzania kuwa na amani na utulivu.
Alisisitiza kazi ya kutunga katiba ni ya wananchi wote. Alisema ni halali watu walio nje kuendelea kutoa maoni yao na misimamo tofauti kwani  baadaye maoni yanachukuliwa na kuchaguliwa yale yanayofaa na yasiyofaa.
Akisihi wajumbe kutumia vizuri nafasi hiyo ya kuwakilisha wananchi, Ngeleja alisema Watanzania wataendelea kuwahukumu kulingana na kile wanachofanya  kwani wajumbe wa Bunge Maalumu ni mawakala wa mabadiliko.
Alisisitiza Tanzania Kwanza haina nia ya kukwamisha mchakato huo na akashauri wadau wote kuendelea kupaza sauti zao.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 4576

Trending Articles