Quantcast
Channel: ziro99blog
Viewing all articles
Browse latest Browse all 4500

KURA YA SIRI, UWAZI YAENDELEA KUWACHANGANYA WAJUMBE DODOMA...

$
0
0
Profesa Ibrahim Lipumba akichangia kuhusu upigaji wa kura bungeni.
Watu wenye busara watatumiwa na Bunge la Katiba kuamua mambo yote yatakayoleta mvutano, ili kuepusha wajumbe wa Bunge hilo kupasuka vipande.

Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Kiongozi Upinzani, Freeman Mbowe, Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Zanzibar Vuai Ali Vuai na Mwenyekiti CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba, wote kwa pamoja walisema utaratibu huo utasaidia kudumisha umoja miongoni mwa wajumbe hao.
Pinda alisema katika hoja hiyo kwamba ili kupata katiba nzuri, wajumbe waepuke kutoa lugha za dhihaka zitakazokasirisha wajumbe hali ambayo inaweza kufanya Bunge hilo lisifikie lengo lake la kutunga Katiba.
Mbowe kwa upande wake, alitaka wajumbe wawe na dhamira njema na kila upande uvumilie upande mwingine, kwani kushindana kwa wingi na kupuuza upande mwingine hakusaidii Tanzania kuwa na Katiba nzuri.
Mbowe alisema kwa sasa ndani ya Bunge hilo, kunaonesha kutoaminiana na baadhi ya wajumbe wameanza kujihusisha na vitendo ya rushwa jambo ambalo alisema watalivunjia heshima Bunge hilo la Katiba.
Profesa Lipumba kwa upande wake alisema Katiba itakayoundwa iwe ile inayowaridhisha wananchi wa pande zote za Muungano. Alisema wajumbe wa Bunge hilo wamekwenda Dodoma kwa ajili ya nchi kupata Katiba mpya na sio maandalizi ya chama fulani kupata kura nyingi uchaguzi ujao.
Vuai pia alikubaliana na hoja ya mambo yote yenye utata yakajadiliwe na Kamati maalum  ya watu wenye busara, lakini akawaonya wajumbe hao kuwa watambue kuwa wametumwa katika Bunge hilo kwa ajili ya kupata katiba itakayodumisha Muungano.
Wakati huo huo, baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba, wameishutumu Kamati ya Kanuni za Bunge hilo, kuwa imeingiza maoni inayotaka yenyewe kwenye vipengele vya rasimu ya kanuni hizo.
Wabunge hao wametaja miongoni mwa vipengele hivyo   kuwa ni upigaji wa kura kuamua ya siri wakati makubaliano ni kuliachia Bunge kuamua kama kura hiyo iwe ya siri au wazi.
Kamati hiyo ya kumshauri Mwenyekiti wa muda wa Bunge kuhusu kanuni za Bunge, ilidaiwa kuingiza baadhi ya maoni ya wajumbe maarufu, maprofesa na madaktari ya kuacha maoni ya wengine wasiokuwa na hadhi hizo.
Mmoja wa wajumbe hao, Peter Serukamba, alisema Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Kanuni, Profesa Costa Mahalu aliyefanya majumuisho ya kanuni hizo, alisema kipengele cha upigaji kura kuwa uwe wa wazi au wa siri anawaachia wajumbe wa Bunge kuamua, lakini katika rasimu waliyopewa inaonesha uamuzi umefikiwa kuwa kura hiyo itakuwa ya siri.
Suala hilo la upigaji kura liliibuka tofauti kubwa bungeni hapo wiki iliyopita, huku kukiwa na taarifa kuwa msimamo wa wabunge na wanachama wa CCM walitaka upigaji wa kura uwe wa wazi.
"Mwenyekiti kifungu cha 37 na 38 tuliambiwa tunaachiwa sisi wajumbe tuamue lakini humu (kwenye rasimu), kamati imeshaweka uaamuzi. Kuna watu kwenye Kamati wanaweka wanayotaka wao,Ó" alisema Serukamba ambaye ni mbunge wa Kigoma Mjini.
Katika rasimu hiyo kifungu cha 37 kinaelezea utaratibu wa kufanya uamuzi ambao unampa mamlaka Mwenyekiti kuhoji Bunge Maalum, ali kupata uamuzi utakaotokana na wajumbe wengi.
Kwa mujibu wa rasimu hiyo, ili rasimu ya Katiba au ibara yake  ipite, italazimu kuungwa mkono na kwa wingi wa theluthi mbili ya idadi ya wajumbe wote kutoka Tanzania Bara na idadi kama hiyo kwa Tanzania Zanzibar.
Kifungu cha 38 kinaelezea kura ya siri kuwa ndiyo itatumika, ambapo kila mjumbe wakati wa kupiga kura atapiga ndiyo au hapana kwa kutumia karatasi ya kupigia kura zitakazoandaliwa na katibu wa bunge maalum.
Naye mjumbe kutoka kundi la walemavu, Vicent Mzema alisema; "mlituambia tulete taarifa za maandishi hamkuzitumia, badala yake mliangalia watu maarufu, maprofesa na madaktari sasa mnatuhakikishiaje tukiandika kwa maandishi taarifa mtaziingiza kwenye kanuni?"
Mzema alitoa kauli hiyo baada ya Mwenyekiti wa muda, Pandu Ameir Kificho kuwataka wajumbe kuwasilisha kwa maandishi, marekebisho wanayotaka yaingizwe kwenye rasimu kwa Kamati ya Kanuni.
Hata hivyo, utaratibu huo ulipingwa na baadhi ya wajumbe waliotaka kujadiliwe bungeni kwa kuzungumza huku wengine wakitaka kwanza kuamuliwe upigaji kura kama utakuwa wa siri au wazi kwa kupiga kura bungeni na si kuandika. Hata hivyo suala hilo halikujibiwa na wajumbe hawakupiga kura hiyo katika kipindi cha asubuhi.
Naye Fahmi Dovutwa kutoka kundi la wanasiasa, alisema rasimu hiyo ya Kanuni imezingatia maoni ya makundi makubwa na kutaka makundi madogo yapewe nafasi.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 4500

Trending Articles