Quantcast
Channel: ziro99blog
Viewing all articles
Browse latest Browse all 4500

UFUNGUZI WA BUNGE MAALUM LA KATIBA BADO KITENDAWILI...

$
0
0
Ukumbi wa Bunge Maalum la Katiba mjini Dodoma.
Mpaka sasa haijulikani lini Bunge Maalum la Katiba, litafunguliwa rasmi, kutokana na kuendelea kusogezwa mbele kwa shughuli muhimu za Bunge hilo kabla ya kufunguliwa kwake.

Awali ilitarajiwa kwamba Rais Jakaya Kikwete angefungua Bunge hilo kwa kulihutubia Februari 24, lakini ilisogezwa mbele mpaka Februari 28 na sasa haijulikani lini litafunguliwa.
Wajumbe hao walikutana katika ukumbi wa Bunge Dodoma kwa mara ya kwanza Jumanne ya Februari 18 na tangu wakati huo, ratiba imekuwa ikivurugwa na shughuli muhimu kuwekwa kiporo.
Baada ya kuvurugwa kwa ratiba hiyo, sasa Bunge hilo limeendelea kusogeza kazi zake mbele, kutokana na   kuchelewa kupitishwa kwa Kanuni za Bunge, ambazo zimeendelea kula siku kadhaa.
Kamati ya Kumshauri Mwenyekiti wa Muda kuhusu Kanuni ya watu 20 iliyo chini ya uenyekiti wa Profesa Costa Mahalu na Makamu wake wawili, Mgeni Haji na Magdalena Rwebangira, leo inatarajiwa kurejesha eneo la kura za mwisho la Kanuni hizo, ili wajumbe waamue, zitakuwa za siri au za wazi.
Kutokana na hali hiyo, sasa inatarajiwa kuwa kazi ya kupitisha Kanuni ikikamilika leo, uchaguzi wa Mwenyekiti na Makamu wake, utafanyika kesho, ikiwa ni wiki ya tatu tangu wajumbe wafike Dodoma.
Kama uchaguzi utafanyika kesho na kutokana na viapo vya wajumbe katika ratiba ya awali kuonesha vingefanyika kwa siku tatu, kwa maana hiyo kama siku hizo tatu zitazingatiwa katika ratiba mpya, basi wajumbe wataapa kuanzia Jumatano, Alhamisi na Ijumaa.
Kwa hali hiyo, ni dhahiri ufunguzi rasmi wa Bunge utakuwa Ijumaa ya wiki hii au mwanzoni mwa wiki ijayo.
Tayari baadhi ya wajumbe ,wamepinga Bunge hilo kuendelea kupigwa kalenda na kueleza kuwa hiyo inawafanya wananchi, kuwaona hawana kitu cha maana wanachofanya hapo.
Mjumbe ambaye pia ni Mbunge wa Kuteuliwa na Rais
na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, alilalamikia Kanuni kucheleweshwa na kusema kama wajumbe hao wa Kamati ya Kanuni wameshindwa kazi, waondolewe na watafutwe wengine.
Akizungumza hivi karibuni Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia, aliunga mkono suala la kuchelewa kuandaliwa kwa Kanuni,  akisema ndio mwongozo unaopaswa kuandaliwa kwa umakini.
Alisema kwa bahati mbaya, Rasimu ya Kanuni
Iliyoandaliwa, inachanganya na imeweka vitu vingine ambavyo si vya muhimu na kuwepo kwa Rasimu yenye masuala ya msingi.
Alitoa mfano wa nchi ya Nepal, ambayo alisema
ilichukua siku 90 kuandaa Kanuni, hivyo na kwa kuzingatia muundo wa Serikali kwa maana ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ipo haja ya Kanuni kuandaliwa kwa umakini ili mijadala iende vizuri.
Bunge Maalumu la Katiba lina wajumbe 629, ambao
ni wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na wajumbe 201, waliotokana na makundi mbalimbali katika jamii.
Baada ya Rais Kikwete kuzindua Bunge Maalumu la
Katiba, utafuata uwasilishwaji wa Rasimu ya Katiba, na kuanza kwa mijadala yake, ambayo imepangwa kufanyika hadi ukomo wake, Aprili 30 mwaka huu.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 4500

Trending Articles