![]() |
Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph Warioba. |
Taarifa iliyotolewa jana na Ikulu Dar es Salaam ilisema uamuzi huo ulifikiwa na Rais Jakaya Kikwete kutokana na maombi ya Tume yenyewe.
“Rais Kikwete ameiongeza Tume muda kutokana na maombi ya Tume yenyewe na kwa mamlaka aliyonayo chini ya kifungu cha 8(3) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ameongeza muda wa Tume hiyo kufanya kazi kuanzia Desemba 16 hadi Desemba 30,” ilisema taarifa.
Hiyo inakuwa ni mara ya pili kwa Rais Kikwete kuiongeza Tume hiyo muda wa kufanya kazi yake.
Kutokana na maombi ya kwanza, Rais Kikwete aliiongeza muda wa siku 45 kuanzia Novemba mosi hadi Desemba 15.
Chini ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Tume hiyo inatakiwa kufanya kazi kwa miezi 18 ambapo pia sheria hiyo inampa Rais mamlaka ya kuiongeza Tume hiyo muda wa kufanya kazi usiozidi siku 60.
Kwa uamuzi wake wa kuiongeza Tume hiyo siku zingine 14, Rais Kikwete atakuwa ameiongeza muda wa kufanya kazi wa jumla ya siku 59 kati ya 60 ambazo anaruhusiwa kisheria kuiongeza.