![]() |
Wanafunzi wakijipatia chakula shuleni. |
Hayo yaliibuka katika kikao cha Baraza la Madiwani la Manispaa ya Sumbawanga mwishoni mwa wiki mjini hapa.
Shule zilizofungwa ni sekondari za Kantalamba, Sumbawanga na Kizwite, ambapo wazabuni hao wamesitisha shughuli zao kushinikiza walipwe madeni yao ya tangu Oktoba.
Wakichangia kwenye kikao hicho baadhi ya madiwani walitaka kujua lini shule hizo zitafunguliwa na nini hatima ya wazabuni hao ambao wamekuwa wakisambaza chakula katika shule hizo.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi umebaini kuwa wanafunzi wa vidato vya pili na nne walimudu kufanya mitihani yao ya kitaifa hivyo waliokumbwa na kadhia hiyo ni wa vidato vingine.
Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, William Shimwela alikiri wazabuni hao kuacha kusambaza vyakula katika shule hizo kwa sababu hawajalipwa malipo yao kutokana na kuchelewa kufika kwa fedha.
"Naomba Baraza hili deni la wazabuni hawa liletwe kwenye Kamati ya Fedha ili kujadiliwa na kupatiwa ufumbuzi," aliomba Shimwela.
Baadhi ya madiwani walionesha masikitiko yao kwa mji wa Sumbawanga kupoteza umaridadi wa siku za nyuma kutokana na kukithiri kwa ujenzi holela unaofanywa na wakazi siku za karibuni.
Walieleza kuwa dosari hiyo imesababishwa na Manispaa ya Sumbawanga kushindwa kugawa viwanja vipya vya ujenzi kwa muda mrefu kutokana na sababu mbalimbali.
Shimwela alisema tatizo la kutogawiwa kwa viwanja vipya linatokana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi kushindwa kupitisha ramani mpya za maeneo ambayo yamekwishapimwa.
Alisema takribani miaka mitatu sasa wamekuwa wakipeleka ramani za maeneo ambayo yalishapimwa ili ziidhinishwe kabla ya wananchi kuanza kujenga, lakini hakuna kilichofanywa na Wizara husika.
"Hii inasikitisha kwani mji huu ulianza kujengwa kwa mpangilio mzuri lakini hivi sasa wananchi wanajenga nyumba ovyo na hii inatokana na kukata tamaa baada ya kusubiri kwa muda mrefu uamuzi wa Wizara husika kupitisha ramani za viwanja vya ujenzi", alisema Shimwela.