Quantcast
Channel: ziro99blog
Viewing all articles
Browse latest Browse all 4503

SERIKALI YAAHIDI NEEMA YA CHAKULA TANI 14 MWAKA 2013/14...

$
0
0
Mizengo Pinda.
Serikali imesema nchi itakuwa na chakula cha kutosha kwa asilimia 118 kwa kuwa na tani milioni 14.4 kwa mwaka 2013/2014, ikilinganishwa na mahitaji ya tani milioni 12.1 za mazao ya nafaka na yasiyo ya nafaka kwa mahitaji ya chakula.

Hata hivyo, pamoja na uhakika huo wa chakula ambao ni sawa na ongezeko la tani milioni 2.2, imesema Halmashauri 61 nchini zinatarajiwa kuwa na uhaba wa chakula.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema hayo jana bungeni mjini hapa, alipokuwa akisoma hotuba ya kuahirisha Bunge la 10 na Mkutano wa 13 wa Bunge.
Alisema hali hiyo inatokana hatua ya upatikanaji wa chakula nchini hadi kufikia Oktoba mwaka huu kuwa ya kuridhisha kufuatia mavuno mazuri ya msimu wa kilimo wa mwaka 2012/2013, ambapo mazao yake yanaendelea kuingia sokoni kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Pinda alisema tathimini ya awali iliyofanyika Julai na Agosti mwaka huu, inaonesha kuwa uzalishaji wa mazao ya chakula katika msimu wa kilimo wa 2012/2013 utafikia tani 14.4.
“Tathmini hiyo inaonesha uzalishaji wa mazao ya chakula kwa msimu wa kilimo wa 2012/2013, utafikia tani hizo ikiwa tani milioni 7.6 za mazao ya nafaka na tani milioni 6.8 za mazao yasiyo ya nafaka.
Hii ni ongezeko la tani milioni 2.2 za chakula ikilinganishwa na mahitaji ya chakula kwa mwaka 2013/2014 ya tani milioni 12. 1 sawa na asilimia 118,” alisema Pinda.
Kuhusu halmashauri zitakazokuwa na uhaba wa chakula, Pinda alizitaja kuwa ni Manyara, Shinyanga, Simiyu, Arusha, Dodoma, Lindi, Tanga, Singida, Mara, Morogoro, Kilimanjaro, Mwanza, Pwani, Mtwara, Kigoma na Tabora.
“Natoa wito kwa Halmashauri zinazohusika katika mikoa hiyo kufuatilia kwa karibu utaratibu wa kupata chakula kinachotolewa kutoka maeneo yenye ziada na kuhakikisha kinafika mapema kwenye maeneo yao kabla ya wananchi wa maeneo hayo hawajaanza kulalamika,” alisema Pinda.
Aidha, alisema serikali inaendelea na tathmini ya kina ya hali ya chakula na lishe katika halmashauri hizo 61 kwa lengo la kubainisha idadi ya watu wenye uhaba wa chakula ili kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa tatizo hilo.
“Nitumie fursa hii kuwaagiza Wakuu Mikoa na Wilaya kuwahimiza wakulima hasa walioko katika maeneo yenye chakula cha ziada kuhifadhi chakula cha kutosha kwa mahitaji ya kaya zao,” alisema Waziri Mkuu.
Pia, aliwataka Wakala wa Taifa na Hifadhi ya Chakula kujipanga vizuri kuhamisha chakula kutoka maeneo yenye ziada na kupeleka kwenye maeneo yenye hali tete ya uhaba wa chakula.
Waziri Mkuu alisema Serikali imebaini kilio kikubwa cha wakulima kuhusu mbolea ni kuwafikia kwa wakati na gharama kubwa.
Alisema kwa sasa mbole ya Minjingu Mazao ambayo awali ilikuwa na matatizo sasa imeboreshwa kwa kiwango kikubwa na kuongezwa virutubisho.
“Mbolea ya Minjingu ya awali ilikuwa na virutubisho vya udongo viwili tu ambavyo ni Kalsiamu na Fosfeti.
Mbolea ya Minjingu Mazao imeboreshwa kwa kuongezwa virutubisho vine na kufanya kuwa sita hivyo inatumika kwa aina nyingi za udongo tofauti na awali,” alieleza Pinda.
Alisema hivi sasa mbolea hiyo ni ya chengachenga tofauti na awali ilivyokuwa ya unga na haikuwa rafiki kwa mkulima na kuongeza kuwa bei ya mbolea hiyo kwa mfuko mmoja ni Sh 32,000 ikilinganishwa na Sh 75,000 kwa mbolea ya DAP.
Kuhusu mbegu bora, Pinda alisema ili kuwawezesha wakulima kutumia mbegu bora (de-linted), Serikali imetoa ruzuku ya Sh bilioni 4.8 ili kufanya mbegu hiyo ipatikane kwa Sh 600 kwa kilogramu kwa mkulima badala ya Sh 1,200 kwa kilogramu iliyotumika mwaka 2012/2013.
Kuhusu Gesi Asilia, alisema Serikali inaandaa Rasimu ya Sheria ya Gesi baada ya kupitishwa kwa Sera ya Gesi Asilia Oktoba 10 mwaka huu ili kuhakikisha miradi ya gesi inatekelezwa kwa manufaa ya Taifa.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 4503

Trending Articles