Quantcast
Channel: ziro99blog
Viewing all articles
Browse latest Browse all 4630

MWANASHERIA ATAKA MUUNGANO KWENYE RASIMU UJADILIWE ZAIDI...

$
0
0
Jaji Mark Bomani.
Mwanasheria Mkuu mstaafu na Jaji Mark Bomani amekosoa Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, akisema ina baadhi ya upungufu hasa katika suala la Muungano.
Akifafanua, amesema mapendekezo ya Tume hiyo hayakuingia ndani kwa kuwa wajumbe hawakupata maoni ya kutosha kwa wananchi na hasa wa Zanzibar na kwamba yaliyosikika ni ya viongozi ambao wengine wanataka Muungano na wengine hawautaki.
Amesema: "Nafikiri ni muhimu kuangaliwa upya Muungano na hasa kwa Zanzibar, waulizwe kwa kupiga kura kabisa kama wanautaka au hawautaki na wanaoutaka uwe wa serikali ya aina gani."
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Jaji Bomani alisema suala la uharaka ifikapo mwaka 2015 Katiba iwe imepatikana, haoni ni wa nini kwani ni vizuri ipatikane Katiba  timilifu na isiyo na dosari.
"Nimeona ni wajibu wangu kutoa maoni katika jambo hili, sasa ni wakati mwafaka wa kukamilisha jambo hili la Muungano maana limezunguka miaka mingi sana," alisema Bomani.
Alisema imechukulia kuwa serikali tatu zinakubalika katika Rasimu kabla hata haijaamuliwa na wananchi na kuhoji kwa nini usipatikane kwanza mwafaka kuhusu shirikisho ndipo mipango mingine ifanyike.
"Ukianza kuzungumzia mgawanyo huu wa madaraka kabla ya kukubaliwa shirikisho  si sahihi, kwa nini tusipate kwanza shirikisho ndipo tupange mabunge yatakuwa mangapi, yatakuwaje na washiriki ni akina nani, hii ni sawa na kuweka farasi nyuma ya mkokoteni," alisema Jaji Bomani.
Alisema ili kupata maoni ya Muungano, wananchi waseme kupitia kura huru na wengi wakikubali ndipo aina ya Muungano na Serikali zake ufikiriwe na ikitokea Muungano umekataliwa na wengi, nchi zigawanywe zibaki na ushirikiano wa kibiashara.
Alibainisha kuwa ni muhimu upatikane Muungano kwa maoni ya wengi kuukubali, ndipo ziundwe Serikali hizo tatu, tofauti na sasa ambapo haijulikani lini wananchi walitoa maoni ya  Muungano huu na mgawanyo wa madaraka.
Aidha, alisema kuna baadhi ya mambo ambayo yanamchanganya katika Muungano, akitolea mfano wa kauli ya Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad ambaye alisema katika Muungano kila nchi iwe na uraia wake, ambapo Jaji Bomani alisema kama kila nchi itakuwa na uraia wake hakutakuwa tena na Muungano.
"Unaposema suala la uraia liwe la nchi si Muungano kama alivyosema Maalim Seif, ina maana Mzanzibari hatamiliki ardhi Bara na wa Bara vivyo hivyo … uraia uwe wa jumla," alisema. 
Alisema badala ya tume au kamati kushughulikia masuala ya Muungano, wananchi wenyewe waachwe waushughulikie na yeye anakubaliana na Serikali tatu; ya Zanzibar, Tanganyika na  ya Muungano.
"Mimi sipendi kuita Tanzania kama wenzetu wanavyoita Zanzibari, kwa nini sisi tuone aibu kuita Serikali ya Tanganyika?" alihoji Bomani.
Alisema aliwahi kutoa ushauri ambao anausimamia, kwamba suala la Muungano ndilo kubwa kuliko yote,  hivyo ipigwe kura ya maoni ya wananchi hasa wa Zanzibar kuuhusu.
"Kwa maoni yangu, Serikali tatu zinafaa ingawa watu wanaogopa, wanaona ni mzigo na gharama, suala la gharama lisiwe kikwazo cha kuundwa au kutoundwa muungano wa serikali tatu," alisema Jaji Bomani.
Kuhusu mapendekezo ya mawaziri na spika kutokuwa wabunge, anakubaliana nayo na kuongeza kuwa hata akiwa na nyadhifa hizo, basi baada ya uteuzi wa spika au waziri aache ubunge.
"Tusiishie tu kwamba mtu akiwa mbunge asiwe waziri au spika, ili kutoa nafasi kwa rais kuteua ndani na nje ya Bunge watu wanaoweza kumsaidia majukumu yake aweze kuteua popote na baada ya uteuzi, ndipo mtu huyo aachie ubunge," aliongeza Jaji Bomani.
Hata hivyo, Jaji Bomani alisema dira ya nchi haijatajwa kwenye Rasimu na ni vizuri itamkwe ili kuepusha viongozi watakaoingia madarakani kubadili watakavyotaka wao.
Alisema dosari nyingine isemwe wazi kwenye Katiba kuwa Tanzania ni nchi ya Ujamaa na Kujitegemea na ieleze ni wa aina gani na pia gharama za elimu ya kiwango fulani isiwepo na iwe hivyo hivyo kwa afya.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 4630

Latest Images

Trending Articles