Quantcast
Channel: ziro99blog
Viewing all articles
Browse latest Browse all 4529

BAJETI YA SERIKALI 2013/14 KUSOMWA LEO DODOMA...

$
0
0
Dk William Mgimwa.
Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa leo anatarajiwa kuwasilisha bajeti ya Serikali ya mwaka ujao wa fedha huku wananchi wakisubiri kuona dhamira yake ya kuwapunguzia ukali wa maisha.
Bajeti ya Serikali ya Sh trilioni 17.7 itasomwa leo saa kumi alasiri wakati asubuhi Waziri wa Ofisi ya Rais (Uhusiano), Steven Wasira, atawasilisha hali ya uchumi na mipango ya Taifa.
Hotuba ya Wasira itaweka sura ya bajeti ya Serikali kwa kuainisha vipaumbele vya Taifa ambavyo viko kwenye mpango wa Taifa wa miaka mitano na utekelezaji wake kwa mwaka wa fedha unaomalizika mwezi huu.
Wasira kwa sasa ndiye waziri anayesimamia Tume ya Mipango ambayo utendaji wake unasimamiwa na Ofisi ya Rais. Mtendaji Mkuu wa Tume hiyo ni Phillip Mpango.
Kwa kuwa tayari wizara zote zimeshaainisha makadirio ya matumizi yao na kupitishwa, kinachosubiriwa sasa ni kuona mipango ya Serikali ya kumpunguzia ukali wa maisha mwananchi wa kawaida, ikiwa ni pamoja na kupunguza kodi katika bidhaa mbalimbali.
Mara nyingi bidhaa zinazofanyiwa marekebisho ya kodi huwa ni vinywaji, sigara, ushuru wa mafuta ya kuendeshea mitambo na petroli, mafuta ya taa na dizeli.
Kuanzia Ijumaa iliyopita hadi jana, tayari kumeanza kufanyika vikao vya kushauriana kati ya Serikali na Kamati ya Bajeti ya Bunge na hatimaye kufanya majumuisho kuzingatia  hoja zenye maslahi kwa Taifa zilizojitokeza wakati wa kujadili bajeti za wizara.
Miongoni mwa mambo ambayo wananchi watahitaji kusikia kwenye bajeti hiyo ni ahadi ya Serikali ya kupunguza kodi kwenye mishahara ya wafanyakazi(PAYE) ambayo imekuwa kilio cha muda mrefu cha wafanyakazi kupitia vyama vyao.
Akihutubia Taifa Mei Mosi jijini Mbeya, katika Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani, Rais Jakaya Kikwete, alisema Serikali yake imesikia kilio cha wafanyakazi na kuwahakikishia kuwa mwaka huu itashusha kiwango cha kodi ya mshahara.
Hata hivyo, Rais Kikwete hakutaja kiwango kipya, badala yake alisema Dk Mgimwa, atatoa ufafanuzi wa suala hilo katika hotuba yake ya bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2013/14.
Mapendekezo ya vyama hivyo ni kutaka kiwango cha kodi wanachokatwa wafanyakazi kibaki tarakimu moja tofauti na sasa ambapo wamekuwa wakikatwa kiasi kikubwa hadi tarakimu mbili kulingana na kiasi anachopokea mfanyakazi.
Maeneo mengine ambayo Serikali imeshauriwa ni kuacha kutoa misamaha ya kodi isiyo ya lazima na ipunguze posho na tofauti ya mshahara wa kima cha chini na cha juu ili iweze  kulipa mshahara wenye tija kwa wafanyakazi.
Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) wakati wa Mei Mosi ilishauri Serikali ipunguze misamaha ya kodi hadi asilimia moja ya pato la Taifa, hatua ambayo itaokoa zaidi ya Sh bilioni 600 kwa mwaka. Kwa hali hiyo hotuba ya Dk Mgimwa itafafanua suala hilo.
Tucta inaamini kuwa Serikali ikizingatia ushauri huo na kuutekeleza, itafanikiwa kuokoa mabilioni ya fedha ambazo zinatumika bila kujali maslahi ya Taifa na zikiingizwa katika bajeti ijayo, zitaboresha mishahara ya wafanyakazi, kuwapunguzia mzigo wa kodi ya mapato na kuboresha pensheni kwa wastaafu.
Licha ya kupunguza kodi hiyo, wananchi pia wanatarajia kusikia wigo mpana wa kodi ukitekelezwa na Serikali katika kutoza kodi huduma za kutuma na kupokea pesa kwa simu za mkononi.
Huduma hizo ambazo kwa sasa zinatolewa na M-pesa, Tigopesa, Airtel Money na Easy Pesa hazitozwi kodi yoyote na tayari Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ameainisha eneo hilo kuwa ni muhimu kutozwa kodi.
Katika kupanua kodi hiyo, pia CAG alishauri kumbi za harusi ambazo kwa sasa ni nyingi mijini nazo zitozwe kodi kwa vile zinaingiza fedha nyingi lakini wamiliki wamekuwa hawatozwi kodi yoyote.
Mjadala wa bajeti hiyo unatarajiwa kuchukua siku saba kuanzia Jumatatu, ambapo michango   inatarajiwa kutolewa na wabunge, na Watanzania watakuwa na hamu ya kujua katika mwaka ujao wa fedha, Serikali imepanga nini kuwaletea maendeleo.
Sura ya bajeti ya leo imelenga kutekeleza vipaumbele vya Taifa kwa lengo la kufikia Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2015. Vipaumbele ni nishati ya umeme, kuboresha miundombinu ya bandari na reli, kilimo, utafutaji mapato, elimu na maji.
Bajeti ya mwaka 2012/13 ililenga kukabiliana na changamoto za uchumi ikiwa ni pamoja na kuongeza fursa za kukuza uchumi, kushughulikia uhaba wa chakula, kupambana na mfumuko wa bei, kuendelea kuimarisha ukusanyaji mapato na kusimamia matumizi na  kushughulikia ukosefu wa ajira hasa kwa vijana.
Bajeti hiyo pia ililenga kuwekeza katika miundombinu ya nishati ya umeme hususan ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam, barabara, bandari na reli ya kati ili kupunguza gharama za biashara na kuongeza tija katika uzalishaji; pia kulipa madeni ya ndani na nje.
Kwa kuzingatia sera za uchumi pamoja na misingi na sera za bajeti, Serikali ilitarajia kukusanya Sh trilioni 15.1. Makusanyo yasiyo ya kodi ya jumla ya Sh trilioni 8.7 (Asilimia 18 ya Pato la Taifa). Mapato kutokana na vyanzo vya halmashauri Sh  bilioni 362.2 (sawa na asilimia 0.7) ya Pato la Taifa.
Washirika wa Maendeleo walitoa misaada ya Sh trilioni 3.2. Kati ya fedha hizo, Sh  bilioni 842.5 ni misaada na mikopo ya kibajeti na Sh trilioni 2.3 ni mikopo na misaada kwa ajili ya miradi ya maendeleo ambayo ilijumuisha Mfuko wa Pamoja wa Washirika wa Maendeleo (Basket Funds) na fedha za Millennium Challenge Account (MCA –T).
Serikali ilikopa Sh trilioni 2.9 kutoka vyanzo vya ndani na nje kuziba pengo la mapato.  Kwa utaratibu wa Serikali, kiasi hicho chote Sh trilioni 15.1 zilitumika ikiwa ni pamoja na Sh  trilioni 10.6 kwa matumizi ya kawaida na Sh  trilioni 4.5 matumizi ya maendeleo.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 4529

Trending Articles