Quantcast
Viewing all articles
Browse latest Browse all 4550

JUKWAA LA KATIBA RUKSA KWENDA KORTINI KUZUIA MCHAKATO...

Image may be NSFW.
Clik here to view.
Jaji Joseph Warioba.
Tume ya Mabadiliko ya Katiba imesema haizuii mwananchi, asasi au taasisi kufungua kesi mahakamani kupinga au kuzuia mchakato unaoendelea wa Katiba Mpya.

Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph Warioba ametoa ufafanuzi huo kwa baadhi ya waandishi wa habari waliofika ofisini kwake Dar es Salaam jana, kutaka ufafanuzi wa masuala yaliyotolewa na Jukwaa la Katiba Dar es Salaam juzi.
Katika tamko lake, Jukwaa la Katiba lilieleza nia ya kufungua kesi Mahakama Kuu ya Tanzania ndani ya siku saba ili kusimamisha mchakato wa Katiba Mpya kutokana na lilichodai ni kasoro zinazojitokeza katika mchakato unaoendelea.
Jaji Warioba alisema Tume haina tatizo na mtu au asasi kwenda mahakamani kwa kuwa hiyo ni haki ya kikatiba.
“Nimesoma tamko lao na niseme tu halina jipya. Hii si mara ya kwanza kusikia hili (la kwenda mahakamani), na jibu letu lilikuwa waende na ndilo jibu letu hadi sasa,” alisema.
“Mimi nasema waende ili tujue Jukwaa hasa ni nani, kwa sababu ninafahamu ni mkusanyiko wa asasi  na baadhi yao zimetuletea maombi ya kuunda mabaraza ya Katiba ya Taasisi na Asasi… sasa jukwaa hili ni nani hasa?,” alisema Jaji Warioba anayeongoza Tume hiyo iliyoanza kazi Mei 2 mwaka jana.
Kuhusu marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Warioba alisema ingawa marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba si jukumu la Tume, wanajua kuwa Serikali ipo kwenye mchakato wa kurekebisha sheria hiyo kama ilivyoahidiwa.
“Hili la marekebisho ya sheria ingawa si jukumu letu, lakini nalo si jipya. Wote tulimsikia Waziri Mkuu hivi karibuni bungeni akisema Serikali inaandaa marekebisho ya Sheria hiyo yatakayowasilishwa bungeni … sasa hawa wanataka nini?” alihoji.
Kuhusu mchakato wa Katiba kukosa uongozi madhubuti, Mwenyekiti huyo alisema Tume yake imeundwa na watu wenye sifa, weledi na uadilifu mkubwa ambao wametokana na mapendekezo ya wadau yakiwamo makundi, vyama, asasi za kijamii na kiraia.
“Mimi najivunia kuongoza Tume yenye watu wenye weledi na uadilifu mkubwa na wananchi wanalifahamu hili na kwa kweli wanatuunga mkono,” alifafanua Jaji Warioba. 
Katika mahojiano hayo, Jaji Warioba pia alifafanua kuhusu muda ambao Tume yake inatarajia kutoa Rasimu ya Katiba kwa lengo la kujadiliwa na kutolewa maoni katika mabaraza ya Katiba.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, hivi sasa Tume inaendelea kuandaa Rasimu ya Katiba na wananchi watapata muda wa kutosha kuijadili na kutoa maoni yao.
“Mpango wa Tume ni kukamilisha kazi zake ndani ya muda uliopangwa na sheria ... tutatoa Rasimu ya Katiba katika muda ambao utatosha kufanya wananchi na wajumbe wa mabaraza ya Katiba kuisoma,” alifafanua Jaji Warioba.
Jaji Warioba pia alielezea kushangazwa kwake na kauli za wadau kuhusu utendaji kazi wa Tume na kusisitiza kuwa wananchi na wadau wengine wasubiri Rasimu ya Katiba itolewe na Tume ndipo watoe maoni.
“Nadhani itakuwa sawa tukishatoa rasimu ndipo watu watuhukumu,” alifafanua Mwenyekiti huyo ambaye pia alishapata kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Kuhusu madai kuwa wananchi waliochaguliwa kuwa wajumbe wa mabaraza ya Katiba ya Wilaya hawana uwezo na weledi wa kujadili na kutoa maoni kuhusu Rasimu ya Katiba, Jaji Warioba alisema madai hayo hayana msingi na yanabeza uamuzi wa wananchi.
Mwenyekiti aliongeza, kuwa uamuzi wa Tume kushirikisha wananchi kuanzia ngazi ya mitaa, vijiji, vitongoji na shehia, ulilenga kuwapa wananchi fursa ya kuchaguana na kuongeza kuwa wananchi walitumia fursa hiyo vizuri.
“Wanaosema haya wanawabeza wananchi waliochagua wajumbe,” alisema Mwenyekiti huyo na kuongeza kuwa taarifa ambazo Tume yake imepata, zinaonesha kuwa katika wajumbe hao kuna wasomi na wenye weledi wa kutosha kujadili Rasimu ya Katiba.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 4550

Trending Articles